VIDEO:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuna faida nyingi za kuunganishwa kwa taasisi za serikali zinazofanya kazi zinazofanana ikiwamo kuondoa urasimu usio na tija na mwingiliano wa majukumu katika nyanja ya udhibiti nchini Tanzania.
Akizungumza leo, Machi 27, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano wa Uhakiki wa Rasimu ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI 2), Prof. Kitila amerejea mifano ya mafanikio ya kuunganishwa kwa taasisi, kama vile kuunganishwa kwa mamlaka za maji na vituo vya kukuza uwekezaji.
Amesisitiza kuwa mfumo uliogawanyika wa taasisi ndogondogo unaunda mazingira magumu ya biashara kutokana na mgongano wa majukumu na gharama zisizo za lazima za kiutendaji. Hivyo, kuna umuhimu wa kubadilisha mtazamo wa kitaalamu kuelekea mfumo wa serikali uliounganishwa unaoupa kipaumbele ufanisi wa kitaifa badala ya kulinda maslahi ya idara moja moja zilizojitenga.